Manufaa ya Ughaibuni na Harakati za Mtaani: Ipi Zaidi?
Manufaa ya kuwa mwanaharakati na kuishi ughaibuni ndio chanzo kikuu cha kufeli kwa harakati hizi. Wanaharakati wengi wa Kitanzania wamekuwa wakihamia ughaibuni kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutafuta uhuru wa kisiasa, usalama, na fursa bora za maisha.
Mfano mzuri ni wakati wa utawala wa Magufuli, ambapo Tundu Lissu alipigwa risasi 16 na timu ya Bashite na kulazimika kukimbizwa nje ya nchi kwa matibabu, huku familia yake ikimfuata. Baada ya Magufuli kufariki, Rais Samia alimfuata Lissu Ubelgiji na kumwomba arudi nyumbani akimhakikishia kuwa hali ya kisiasa imekuwa shwari.
Aliporudi Tanzania, Lissu alipata fursa mpya ya kufanya siasa hadi akazindua kampeni ya "No Reforms, No Elections"—harakati za kuzuia uchaguzi. Mwishowe, Lissu aliishia kukabiliwa na kesi ya uhaini na kushikiliwa na vyombo vya dola. Hata hivyo, familia yake aliiactha Ubelgiji ili iendelee kunufaika na hifadhi ya kisiasa.
Ukweli Kuhusu Maandamano ya 7/7
Hali ya wanaharakati kuishi nje inaleta changamoto kubwa kwa harakati za ndani ya nchi. Wanapokuwa mbali na Tanzania, wanakosa kushiriki moja kwa moja katika mijadala ya kijamii na kisiasa na kushindwa kuzielewa kwa undani kero za wananchi. Wanapotoa wito wa maandamano, mara nyingi hawajitokezi wao binafsi wala familia zao. Hii inaleta taswira ya kutokuwa na mshikamano wa kweli na wananchi wanaoishi Tanzania. Wanaharakati walioko nje—ambao ndio walikuwa viongozi na wachochezi wa maandamano ya 7/7—walibaki kuwa wasemaji tu bila kushiriki hatari wala gharama zinazotokana na maandamano hayo.
"Dada wa Taifa" (Mange Kimambi) na Maria Sarungi walisisitiza kuwa kitendo cha wafanyabiashara kutofungua maduka kilikuwa ni ishara ya kuunga mkono maandamano; kwani kwa kusitisha shughuli zao za kila siku, walionyesha mshikamano na wito huo. Kumbe Mange na Maria Sarungi, kwa sababu ya kuishi Marekani na Kanada, hawakuelewa hali halisi ya Watanzania wa kawaida. Wananchi wengi walihofia vurugu, maafa, na kupoteza mali zao, ndiyo maana hawakufungua maduka.
Athari kwa Wananchi wa Kawaida
Pia, hawakuelewa kuwa vijana wengi wanaishi kwa kipato cha siku kwa siku (cha juu chuma, cha chini keti), hivyo siku hiyo ilitutesa sana. Kumbuka, hapo nyuma walipoanzisha kampeni ya #DontVisitTanzania wakidhani wanakomoa serikali, walioumia zaidi ni sisi waongoza watalii (tour guides), wafanyakazi wa hoteli, wapandisha wageni Mlima Kilimanjaro, pamoja na madereva wa taksi za viwanja vya ndege.
Wanapodai hifadhi ya kisiasa, nchi zinazowapokea mara nyingi huchukua jukumu la kugharamia maisha yao. Hii ni pamoja na kuwalipia kodi za nyumba, chakula, na hata ada za shule za watoto wao. Kwa mfano, katika baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na Marekani, wakimbizi hupatiwa misaada ya kifedha na huduma za kijamii bila gharama yoyote. Hii huwapa motisha ya kubaki ughaibuni kwa muda mrefu badala ya kurudi Tanzania kushiriki moja kwa moja katika harakati za kijamii na kisiasa.
Ndio maana kuna wanaharakati wengine—ambao Dada wa Taifa, Mange, huwa awaita "uchwara"—wanajiunga na harakati hizo lakini kazi yao kubwa inakuwa ni kutukana tu ili kupata fursa za kimaisha.
Hitimisho
Kwa ujumla, tatizo la wanaharakati kuishi ughaibuni badala ya Tanzania linatokana na mchanganyiko wa masuala ya usalama, fursa za elimu kwa familia zao, na msaada wa kifedha wanaoupata huko nje. Hata hivyo, hali hii inadhoofisha nguvu ya harakati za ndani na kuwaacha Watanzania wakikabiliana na changamoto peke yao bila msaada wa moja kwa moja kutoka kwa viongozi wa harakati hizo.
Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa. Kuwa wa kwanza kuchangia.